Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Katika hafla ya kumbukumbu ya kwanza ya Mashahidi wawili Mashuhuri wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon, Sheikh Nabil Qawuq na Sayyid Suhail Al-Husseini, Sheikh Naeem Qassem alisisitiza juu ya kuendeleza njia ya Muqawama na kulinda mhimili wa haki.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi kadhaa wa Muqawama, Wanasiasa, Wanazuoni wa Dini na familia za Mashahidi.
Kumbukumbu ya Sheikh Qawuq: Kutoka medani za vita hadi usalama wa kujikinga
Katibu Mkuu wa Hizbullah katika hotuba yake alimtaja shahidi Sheikh Nabil Qawuq kama mwenzake wa karibu wa shahidi Sayyid Hashem Safiuddin aliyepoteza maisha yake katika siku kama hiyo mwaka uliopita.
Akitaja nafasi kubwa ya Qawuq katika kukabiliana na vita vya kulazimishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Sheikh Qassem alielezea majukumu yake katika kitengo cha usalama wa kujikinga tangu mwaka 2018 hadi wakati wa shahada yake.
Alibainisha kuwa kukubali jukumu hilo kulifanyika kwa utiifu kamili kwa amri ya Sayyid Hassan Nasrallah.
Alikumbusha pia ushirikiano wa karibu wa Qawuq na wapiganaji katika kusini mwa Lebanon, Beirut na Syria, pamoja na mchango wake katika nyanja za kielimu na kidini. Alitaja kuwa alikuwa na maandiko muhimu katika masuala ya sira, maadili na itikadi.
Shahid Qawuq: Mfano wa ufahamu, imani na kujitolea katika vita moja
Sheikh Naeem Qassem alimuelezea Shahid Qawuq kuwa ni mfano wa ufahamu, imani na kujitolea, akisema:
“Wakati maadui wanapolenga Iran, Muqawama wa Kiislamu na Palestina, yote haya ni sehemu ya vita moja. Kila mmoja katika eneo anapaswa kubeba jukumu lake kwa kadiri ya uwezo wake.”
Akitaja pia kuuawa kwa wanazuoni 12 katika vita vya “Awliyaa’ul-Ba’s”, alisisitiza nafasi muhimu ya wanazuoni katika harakati za kisiasa, kijihadi na kiutendaji za Umma.
Sayyid Suhail Al-Husseini: Mshirika wa Hajj Imad Mughniyah na majukumu ya kiusalama
Katibu Mkuu wa Hizbullah pia alimzungumzia Shahid Sayyid Suhail Al-Husseini, kamanda wa kijihadi, aliyekuwa miongoni mwa wafuasi wa mwanzo wa Hajj Imad Mughniyah katika harakati za muqawama.
Alitaja jukumu kubwa la Hajj Imad katika kutegemea juhudi za kijihadi na kiusalama za Shahid Al-Husseini.
Sheikh Qassem alifafanua majukumu yake ya kiusalama katika eneo la Beirut mwaka 1991, huduma yake kama msaidizi wa Hajj Ridwan, na mapambano yake dhidi ya ujasusi hadi mwaka 2000.
Tangu mwaka 2008, alikuwa msaidizi wa Sayyid Hassan Nasrallah na alijulikana kwa kuzingatia masuala ya kifamilia ya wapiganaji, jambo lililomfanya kuwa mlezi na mwalimu wa kijamii. Pia alipewa jukumu la kushughulikia mgogoro wa kiuchumi na kijamii na alianzisha miradi mingi ya kusaidia wananchi.
Mpango wa “Israel Kubwa”: Mradi wa eneo lote unaoungwa mkono na Marekani
Sheikh Naeem Qassem alieleza kuwa utawala wa Kizayuni unalenga kufanikisha mradi wa “Israel Kubwa” ambao unapata uungwaji mkono kamili kutoka Marekani.
Alibainisha kuwa kila hatua inayoonekana katika eneo ni sehemu ya mradi huo, na hata kurudi nyuma kwa muda ni ujanja wa adui kupata fursa.
Alisisitiza kuwa matukio ya Gaza katika miaka miwili iliyopita ni sehemu muhimu ya mradi huo, na kila kitu katika eneo limeunganishwa.
Akasema:
“Lazima sote tukabiliane na hatari hii; hakuna nchi inayoweza kusema ipo mbali na suala hili, kwani wote wamelengwa. Hatua iliyoanza Gaza leo, kesho itafika kwingine kwa mtazamo wa Kizayuni.”
Mpango hatari wa Trump kwa Gaza: Vazi la Kimarekani juu ya mpango wa Kizayuni
Sheikh Qassem aliuita mpango wa Trump kuhusu Gaza kuwa ni wenye hatari kubwa, na kwamba umepangwa kulingana na maslahi ya Israel.
Alisema kuwa mpango huo wa Kizayuni umevalishwa vazi la Kimarekani, jambo lililoleta maswali mengi hata kwa baadhi ya viongozi wa Kiarabu walioutilia shaka.
Akiurejelea mpango huo, alitaka kujua:
“Ikiwa utakuwepo utawala wa kimataifa Gaza ambao hautaweza kutekeleza wajibu wake, na wapiganaji wa muqawama wakikamatwa, je, ni mafanikio gani yatakayobaki ya mapambano haya?”
Pia alitaja sababu nne za kuwasilishwa kwa mpango huo wakati huu, ikiwa ni pamoja na jaribio la kuisafisha Israel kutokana na wimbi la lawama za dunia na kuupamba uso wake wa kihalifu.
Meli za mshikamano na matarajio ya msimamo wa Wapalestina
Sheikh Qassem alisema kuwa ujio wa meli za kimataifa za mshikamano kutoka nchi zaidi ya kumi kujaribu kuvunja mzingiro wa Gaza ni dalili ya udhaifu wa Israel.
Aliwashukuru hasa watu wa Uhispania kwa msimamo wao wa wazi katika hili.
Akasema kuwa wanangoja matokeo yatakayotangazwa na Wapalestina wenyewe, kwani mpango wa Trump si makubaliano bali ni pendekezo tu.
“Palestina haitasalimu amri,” alisema, “na angalau nchi za Kiarabu na Kiislamu zisitie shinikizo kwa muqawama.”
Onyo dhidi ya njama za adui za kuchochea fitna nchini Lebanon
Katibu Mkuu wa Hizbullah alionya kuwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni yanalenga kuwashinikiza wananchi wa Lebanon na kudhoofisha nchi, kwa msaada kamili wa Marekani.
Alikumbusha pia kushindwa kwa mpango wa Marekani wa kupanua ushawishi wake wa moja kwa moja katika masuala ya eneo.
Sheikh Qassem alisema adui anataka kuchochea migawanyiko ndani ya jeshi la Lebanon, lakini jeshi hilo limeonyesha busara, na pande zote — jeshi na muqawama — zimesema wazi kuwa fitna haitakubalika.
Alikiri kuwa uwezo wa kijeshi wa Hizbullah hauwezi kulinganishwa na ule wa Israel, lakini akaeleza ubora wa muqawama unatokana na uaminifu kwa taifa, kujitolea, na dhamira ya watu.
Urejeshaji wa Mamlaka na Upinzani dhidi ya mipango ya kigeni kuhusu uchaguzi
Sheikh Naeem Qassem alihimiza viongozi wa Lebanon kuendelea kudai kurejesha mamlaka kamili ya nchi na kuunda kamati maalum kwa ajili ya hilo.
Aliwakosoa wanasiasa wanaoendeleza maslahi ya Marekani na Israel, akisema kushughulika na mambo madogo kunapunguza majukumu ya serikali katika masuala muhimu.
Pia alisisitiza haja ya kujenga upya Lebanon na kuitaka serikali kupanga mipango madhubuti ya utekelezaji.
Kuhusu marekebisho ya sheria za uchaguzi, alionya kuwa haiwezekani kuunda sheria kwa manufaa ya kundi maalum na kukataa mipango yote inayotokana na shinikizo za kigeni.
Your Comment